Ida Odinga ambaye ni mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Odinga, ametoa wito wa kuendelezwa kwa urithi wa Raila Odinga.
Akizungumza leo Ijumaa mtaani Karen wakati wa hafla ya uwasilishaji wa kumbukumbu za Raila Odinga kwa familia yake kutoka kwa serikali, Mama Ida alisema marehemu Raila atakumbukwa kila wakati kwa kujitolea na kupambana kuhakikisha kwamba kila Mkenya anaishi maisha ya heshima.
Alidokeza kuwa wageni ambao wamekuwa wakizuru nyumbani kwao miezi kadhaa baada ya kufariki kwa Raila ni dhihirisho tosha kwamba maisha na kazi ya Raila yalikuwa mfano bora kwa wengi.
“Milango yetu iko wazi. Bado tunawapokea wageni na jumbe za heri njema, na hatua hii haitakamilika hivi karibuni,” alisema Ida.
“Sasa kwa kuwa ametuacha, tunapaswa sasa kuendeleza urithi wake kulingana na ndoto zake,” aliongeza Mama Ida.
Ida alisema ombi la Raila kwamba azikwe ndani ya saa 72, ilishangaza familia hiyo, huku akimshukuru Rais William Ruto kuhakikisha ombi hilo limetimizwa.
“kila kitu kilifanywa kwa haraka na tunamshukuru Rais William Ruto, aliyehakikisha ombi la Raila limetimizwa,” alidokeza Ida.
Akiwasilisha kumbukumbu hizo, Katibu wa Wizara ya Mambo ya Korir Sing’Oei, alisema ujumbe huo wa rambirambi ulitambua mchango wa Raila katika sera za kimataifa za Kenya, uwiano wa miundombinu na sauti ya Afrika katika maswala ya kimataifa.
“Alichagua mazaungumzo badala ya migawanyiko, umoja badala ya utengano na suluhu za muda mrefu badala ya maslahi ya kibinafsi,” alisema Sing’Oei.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja familia, marafiki, maafisa wa serikali na wale wa kidiplomasia.
