Francis Meja ateuliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amemteua Francis Meja kuwa mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma – PSC, kulingana na taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Meja kwa sasa anahudumu kama mjumbe wa PSC, wadhifa ambao ameshikilia tangu mwezi Januari mwaka 2025.

Ana uzoefu mkubwa katika sekta ya umma, kwani amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu mwanzilishi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani – NTSA.

Alihudumu pia kama Msajili wa Magari katika Wizara ya Uchukuzi, na mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Murang’a.

Mbali na rekodi yake ya utumishi wa umma, Meja ana zaidi ya miaka 15 ya uzoefu katika sekta ya benki na huduma za kifedha.

Amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali za usimamizi katika benki ya Equity na kampuni ya ufadhili wa nyumba -HFCK.

Ana shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa biashara katika somo la Usimamizi wa Kimkakati kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kwa kuzingatia matakwa ya katiba kuhusu uteuzi wa nyadhifa za serikali, Rais amewasilisha jina la Meja kwa bunge la kitaifa kwa usaili kabla ya kuidhinishwa.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Rais William Ruto alitangaza wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya PSC kuwa wazi na kuteua jopo la wanachama saba la kuteua mwenyekiti mpya.

Website |  + posts
Share This Article