Mwanamuziki wa Uganda Bebe Cool ameamua kumsamehe mtayarishaji wa maudhui wa TikTok, Luwilight, aliyekamatwa hivi karibuni na kuzuiliwa katika Gereza la Luzira kwa tuhuma za kusambaza taarifa potovu na lugha ya chuki.
Katika mahojiano ya simu, Bebe Cool aligusia uamuzi wake wa kumsamehe mtayarishaji huyo wa maudhui mwenye utata, akimpa fursa ya pili ya kujijenga upya kitabia.
Alifichua kuwa Luwilight ataachiliwa hivi karibuni, akimhimizwa kutafakari juu ya matendo yake na kutumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji zaidi siku zijazo.
“Nina binti nyumbani na kudharauliwa mtandaoni, hasa pale kunapoathiri taswira yangu machoni pake, ni jambo ambalo siwezi kupuuza,” Bebe Cool alieleza.
Msanii huyo alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuweka mifano mizuri kwa kizazi kipya.
Luwilight, ambaye alijipata kwenye vichwa vya habari wiki chache zilizopita baada ya kushtakiwa kwa kusambaza taarifa za uongo na lugha ya chuki, alikuwa amenyimwa dhamana alipofikishwa mahakamani tarehe 21 Januari.
Nyota huyo wa mitandao ya kijamii alipelekwa katika Gereza la Luzira baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Anatarajiwa kurejea mahakamani tarehe 2 Februari 2026, huku uchunguzi wa kesi yake ukiendelea.
Bebe Cool pia alizungumzia suala pana la mienendo ya mtandaoni, hasa miongoni mwa washawishi wa mitandao ya kijamii.
“Sote tuna wajibu wa kuheshimiana mtandaoni,” alisema. “Haijalishi uko upande gani wa siasa. Tukumbuke kwamba kuna maisha baada ya siasa.”
